2025.09.22 Padre Matthew Eya aliuawa huko Nigeria 2025.09.22 Padre Matthew Eya aliuawa huko Nigeria 

Padre aliuawa katika shambulizi la kuvizia barabarani kusini mashariki mwa Nigeria

Padre Mathayo Eya alipigwa risasi jioni ya Septemba 19 kando ya barabara ya Eha-Alumonah–Eha-Ndiagu katika Eneo la Serikali ya Mtaa ya Nsukka,Mkoa wa Enugu,kusini mashariki mwa Nigeria.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Shirika la Kipapa la Habari za Kimisionari FIDES, ilibainisha kuwa Padre mmoja aliuawa katika shambulizi la kuvizia kando ya barabara nchini Nigeria. Kulingana na ushuhuda uliokusanywa na vyombo vya habari vya eneo hilo, Padre Eya, ambaye alikuwa Paroko wa Kanisa la Mtakatifu Charles huko Eha-Ndiagu, alikuwa mwathirika wa shambulio la kuvizia kando ya barabara. Padre huyo alikuwa akirejea katika parokia yake wakati watu wawili waliokuwa na silaha wakiwa kwenye pikipiki waliposimama kando ya gari lake, wakifyatua tairi zake. Mara baada ya gari kulazimika kusimama, walimpiga risasi kadhaa karibu.

Jaribio la kulengwa makusudi

Ikiwa hali zilizoripotiwa na mashahidi ni sahihi, halikuwa jaribio la utekaji nyara lililoshindikana bali mauaji yaliyolengwa. Habari za kuuawa kwa padre huyo zilithibitishwa na Monsinyo Cajetan Iyidobi, Chansela wa Jimbo kuu la Nsukka, katika ujumbe wake kwa waamini unaosomeka hivi: “Nimeshtuka sana, kwa uchungu na huzuni, lakini kwa kujisalimisha kabisa kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu na tumaini thabiti la ufufuko wa wafu, ninawataarifu kifo cha kusikitisha cha ndugu yetu mwingine, Padre Mathayo Eya. Polisi wameanzisha msako wa kuwasaka wauaji wa Padre Eya na kuwakamata watu 38 ambao baadhi yao wanashukiwa kuhusika na mauaji hayo.

Utambuzi wa atakayetoa taarifa za wahalifu

Serikali ya Mkoa wa Enogu imeweka zawadi ya naira milioni 10 (kama euro 5,700) kwa atakayetoa taarifa za wauaji wa Padre huyo.

Mauaji ya Padre Mathayo nchini Nigeria
22 Septemba 2025, 10:06