2025.09.09 Ushiriki wa Misa ya kumshukuru Mungu Kutangazwa kwa Karlo Acutis kuwa Mtakatifu,iliyofanyika katika Shule ya KWAUSO,jimbo katoliki, Bukoba Tanzania. 2025.09.09 Ushiriki wa Misa ya kumshukuru Mungu Kutangazwa kwa Karlo Acutis kuwa Mtakatifu,iliyofanyika katika Shule ya KWAUSO,jimbo katoliki, Bukoba Tanzania. 

Pd.Rwehabura:“Vijana tunzeni usafi wa moyo kama Carlo Acutis na ibada ya Maria!

Kumtanguliza Mungu katika kila jambo na kuishimaisha yanayompendeza Mungu na kuabudu Ekaristi Takatifu,kama Mtakatifu Carlo Acutis.Ni ushauri uliotolewa na Padre Rwehabura,Gambera wa Seminari ndogo ya Mtakatifu Don Bosco- Rutabo,Jimbo Bukoba,Tanzania katika Misa ya kushukuru Mungu,kutangazwa Mtakatifu Carlo Acutis,Septemba 7.Na Mkurugenzi wa KWAUSO,Padre Mutajawaha,alisimulia ufadhili kutoka kwa Bi Adriana Acutis,shangazi yake Carlo Acutis akiona maajabu ya Mungu.

Na Patrick P. Tibanga - Radio Mbiu na Angella Rwezaula – Vatican.

Mama Kanisa, tarehe 7 Septemba 2025, amewapata Watakatifu Wapya, Carlo Acutis na Pier Giorgio Frassati, waliotangazwa na Baba Mtakatifu Leo XIV katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, mjini Vatican  kwa ushiriki wa mamia elfu ya waamini kutoka Ulimwenguni kote. Katika tukio hilo liliunganisha makanisa mbali mbali Katoliki Ulimenguni katika kushiriki ibada ya misa takatifu katika maparokia na vituo vyao  mbali mbali vya ibada za shukrani kwa ajili ya watakatifu hao vijana wapya. Miongoni mwake ni katika Kikanisa cha Shule ya Sekondari iitwayo  “Kwa Heshima ya Uso Mtakatifu wa Yesu (KWAUSO),” katika Jimbo Katoliki la Bukoa Tanzania, iliyoongozwa na Padre Valence Rwehabura, Gambera wa Seminari ndogo ya Mtakatifu Don Bosco- Rutabo Jimbo Katoliki Bukoba.

Padre Rwehabura akitoa mahubiri yake
Padre Rwehabura akitoa mahubiri yake

Katika mahubiri yake aliwashauri waamini na wanafunzi walioshiriki misa hiyo  kumtanguliza Mungu katika kila jambo wanalolifanya na kuishi maisha yanayompendeza Mungu na kuabudu Ekaristi Takatifu ili kuurithi uzima wa milele. Padre Valence alisema kuwa, “kila mmoja katika nafasi yake anatakiwa kumtanguliza Mungu katika kila wanayoyafanya ili kuwa watakatifu, kwani Mungu anamuita kila mwanadamu kuwa Mtakatifu lakini kupitia maisha anayoishi, mwadamu hubadilika na kuyaishi maisha yasiyo mpendeza Mungu.” Padre Valence akidadavu juu ya Tukio la siku hiyo ya kutangazwa Watakatifu,  alimfafanua Mtakatifu Carlo Acutis, kijana alivyokuwa na ibada kwa Mama Bikira Maria na kuwahasa vijana kumtanguliza Kristo na Mama Maria katika vikwazo mbali mbali vya maisha wanavyo kumbana navyo.

Wakati wa Misa ya shukrani kutangazwa Carlo Acutis
Wakati wa Misa ya shukrani kutangazwa Carlo Acutis

“Kijana huyu alikuwa na ibada kwa Mama Bikira Maria, alipokuwa katika umri ule wa ujana alikwepa vishawishi vingi ikiwemo kuingia katika mtego wa mahusiano, yeye alimtanguliza Mama Bikira Maria.” Padre Rwehabura alifafanua tena kwa kutoa mifano yake akisema:  “katika maisha yangu binti yangu ni mmoja tu,  ambaye ni Mama Maria” kwa hiyo nawe kijana kwa wadada mseme Yesu ni kijana anayenipendeza kuliko vijana wote na wanaume mseme binti yangu ni Mama Maria. “Aidha aliwakumbusha Wakristo wakatoliki kutenga muda na kuabudu Ekaristi Takatifu na kupeleka mizigo yao kwa Yesu wa Ekaristi, pamoja na kuitumia vyema mitandao ya kijamii kama alivyofanya Mtakatifu Carlo Acutis katika maisha yake.

Wakati wa Misa ya shukrani kwa Mungu
Wakati wa Misa ya shukrani kwa Mungu

Ushuhuda wa Mkurugezi wa KWAUSO

Naye Mkurugenzi wa Shule ya Sekondari ya KWAUSO, Padre Stanslaus Mutajwaha alitoa ushuhuda wa Imani ya kuhusu muujiza wa Mwenyeheri Carlo Acutis hasa katika kumkutanisha  na Shangazi yake Adriana Acutis bila kutegemea  na kushangazwa  kupata msaada wa ujenzi wa Kanisa katika shule hiyo. Na yote hayo alieleza kuwa yalitokana na  sala ya Novena aliyoifanya na Mungu akamwangazia mwanadamu kwa mambo wasiyoyatarajia wala kufikiria. Ni kupitia tafakari yake alifanikiwa kufanya mawasiliano kwa njia ya mtandao na shangazi huyo wa Carlo Acutis na  ambaye alifanikiwa kumchangia Euro 25,000, sawa na zaidi ya Tsh. Millioni 70,  fedha za Tanzania, ambazo ziliwezesha ujenzi wa Kanisa la shule hiyo na baadaye kufanikiwa kuchangia mchango wa jengo la Mapadre katika shule hiyo, litakalojengwa na  ambalo limekewa  jiwe la msingi na Padre Valence Rwehabura baada ya Misa hiyo Takatifu, kwa niaba ya Askofu wa Jimbo Katoliki Bukoba tarehe 7 Septemba 2025, katika ukumbusho  wa siku ya Kutangazwa Watakatifu wapya Carlo Acutis na Pier Giorgio Frassati.

Maelezo kamili ya Padre Mutajwaha kuhusu Carlo Acutis na Sanda ya Torino

Mkurugezi wa Shule hiyo ya KWAUSO, Padre Stanslaus Mutajwaha wakati wa kueleza uhusiano kati ya Shule hiyo na Mtakatifu Carlo Acutis alifafanua kwa kirefu zaidi. Kwa nja hiyoa alianza kwa kuwashukuru wanafunzi, kwa kushiriki kwao siku hii ya kuona rafiki yetu, mwombezi wetu, Carlo Acutis, anaye inuliwa mbinguni, anafanywa kuwa  Mtakatifu. Tulikuwa timezoea kusema mwenyeheri Carlo Acutis, tangu leo hatusemi tena mwenyeheri Carlo Acutis, bali Mtakatifu Carlo Acutis. Ni mabadiliko makubwa tumshukuru mwenyezi Mungu.” Padre Mutajwaha alisema kwamba katika yale ambayo alikuwa ameandaa kuzungumzia kuhusu Carlo Acutis, kwa bahati nzuri Padre  Valence alimefanya vizuri….! Japokuwa alitaka kuengeza kidogo tu yale ambayo binafsi kwa namna flani Padre Valence alikuwa amesema: mnamo mwaka 1991 Carlo Acutis, alizaliwa huko London, tarehe 3 Mei, na kwamba alipokutana na Adriana Acutis,(shangazi yake) anasema: huyu mama ambaye sijawahi kukutana naye macho kwa macho mpaka sasa hivi, nilifurahi sana. Alifika hapa kwa njia ya namna yake, siyo ya mwili lakini, alifika hapa, ametubebea zawadi ya Kanisa hili zuri namna hii. Mimi sijawahi kukutana naye popote lakini alifika hapa kwa njia ya namna yake, nimshukuru Mungu namna gani...!

Mkurugenzi wa Shule ya KWAUSO, Padre Mutajwaha akitoa maelezo
Mkurugenzi wa Shule ya KWAUSO, Padre Mutajwaha akitoa maelezo

Padre Mutajwaha aliendelea kusema: Alifika na kutambulisha kwamba yeye ni shangazi wa Carlo Acutis. Ila mwanzo nilikuwa nimesikia kidogo kidogo juu ya Carlo Acutis, lakini sikuwa najua zaidi. Basi, baadaye nikamuuliza, hivi Carlo Acutis, nimeona kwenye mtandao kwamba, amezaliwa tereh 3 Mei,  hivi, amezaliwa saa ngapi? Kwa sababu nilipo angalia angalia kwenye kalenda niligundua kwamba, hiyo tarehe 3 Mei ilikuwa ni siku ya Ijumaa. Na mwaka huo, kuanzia terehe 8 Agosti 1990, nilikuwa nimefanya Novena kidogo binafsi, …. Ila nilikuwa nataka nifanye Novena ndefu kama ya miezi 9 kusudi kuimaliza  novena hiyo terehe 8 Septemba kama kesho, basi, na nifanye hija yangu huko Lourdes.

Ilikuwa novena binafsi, iliyokuwa inanihusu mimi, na mambo yangu. Wakati huo na  novena yangu, nilikuwa nimepanga kwamba kila Ijumaa,  masaa kadhaa, nifanya kazoezi fulani, kabinafsi, …., na wakati huo nilikuwa Roma. Basi, nilikuwa nakafanya kila Ijumaa, na  nilipogundua kwamba, terehe alipozaliwa, Carlo Acutis, ilikuwa terehe 3 Mei  na hiyo siku ilikuwa Ijumaa, basi, nikatafuta  konekisheni, kusudi  awe na mimi karibu zaidi, na nikamuuliza, je, amezaliwa saa ngapi? Ili nione kama kuna kakonekisheni flani kati ya zoezi langu la binafsi na kuzaliwa kwake, nikagundua kwamba kumbe amezaliwa saa kama moja tu, kabla sijaingia kwenye kale kazoezi. Nilifurahi na kuona kwamba, kumbe mwenyezi Mungu anaweza kupanga mambo yake na kukufanyia konekisheni miaka mingi hata kabla wewe hujajua na hiyo konekisheni inakuja kudhihirika kwenye ujio wa shangazi yake Carlo Acutis mwaka 2022.

Adriana Acutis alimjuaye Padre Mutajwaha?

Padre Mutajwa aliendelea juu ya historia hii. Je alinijuaje huyu mama Adriana Acutis? Alinijua katika kutafakari kwangu juu ya shuka ambalo ni nakala ya shuka lingine linaloitwa  Sanda ya Torino. Nilianza kulitafakari tangu mwaka 1985, na katika kuendelea kuitafakari kuna (picha hapa (mtaiona aliowaelekeza Kanisani),  lakini pia kupitia mtandao mnaweza kujifunza mengi zaidi juu ya hilo.  Basi, nikaendelea kutafakari juu ya jambo hilo na katika kutafakari juu ya jambo hilo nilikuwa na wasiwasi juu ya hii sehemu ya  Kwauso (kijisehemu kidogo ndani ya shule) kimeachwa makusudi na tangu tulipochora ramani ya jengo zima la KWAUSO (shule) kusudi pale tuweze kujenga nyumba ya Mkutano wa Watu  mbalimbali, vile vile iwe nyumba ya Sala. Mnamo  mwaka 2022, nikawaza je, nifanyeje? Kwahiyo Mungu alimleta Adriana. Na jinisi alivyonijua, mimi msiniulize…  ila nilikuwa kwenye kasimu kangu hapo, ninatembea tembea, nikasikia meseji ya whatsapp inaingia, akijitambulisha kuwa yeye ni Adriana na akaniahidi kwamba atanitumia Komputer. Kwa njia hiyo, baadala ya Komputer zenyewe akaniuliza unaonaje nikikutumia pesa? Nikasema ni vizuri zaidi, basi tukafanya mpango kwamba atume pesa, na sikuwa ninajua kwamba ni pesa kiasi gani, na alituma kiasi cha  Euro 25,000.

Mbele ya Kikanisa cha Shule ya KWAUSO
Mbele ya Kikanisa cha Shule ya KWAUSO

Wale wanaojua Euro ni nini, hizo ni pesa nyingi sana kwa pesa za kitanzania, hununui Komputer zinazoharibika harafu uwape wanafunzi waziharibu, basi, nikamuuliza je? Unaonaje nikinunua Komputer kama 10 alafu pesa nyingine itakayobaki nianze kutayarisha kwa ajili ya kujenga ukumbi ambapo tutakuwa tunasalia. Aliniuliza hivi hamna mahali pa kusalia? Nikamjibu hatuna, basi akajibu kwamba fanya hivyo hivyo lakini nitahakikisha nimekusaidia vile vile kujenga mahala pa kusalia. Na  ndiyo hivo nilivyokutana na huyo Adriana Acutis. Ni mipango ya Mwenyezi Mungu  ambayo inakuja wakati sisi tumelala, wakati sisi hatuna la kufikir, i mwenyezi Mungu anafanya konekisheni. Baada ya hapo, ndipo Carlo Acutis akatangazwa kuwa mwenyeheri, alafu baadaye mambo yamekwenda, mbele na  leo ametangazwa Mtakatifu. Ninaona ni jambo kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ni neema tele, na kwa upande wetu anapokuja, anasema msisherehekee tu hivi hivi, bali pamoja na kusherehekea mjueni kwamba ninawatumia chochote. Kwa njia hiyo Padre  Valence tunakuomba baada ya hapa tunakwenda, utuwekee jiwe la msingi kwa  ajili ya nyumba ya mapadre. Hii ni kutokana na ufadhili wa huyo Adriana Acutis, ambaye mimi nanaona ni Baraka kutoka katika maombezi ya huyo Carlo Acutis. Ninamshukuru Mwenyezi Mungu, hata sijui nimshukuru namna gani,  lakini naona alinifanyia makubwa.

Nakala ya Sanda ya Torino
Nakala ya Sanda ya Torino

Nakala ya Sanda ya Torino

Na hiyo nyumba itaitwa Veronica, kwa sababu, huyo mama Adriana alivyokuja kunijua alinikuta katika hii mitandao, siku moja mnamo  mwaka 2020, wakati  ule wa katikati ya Uviko 19. Watu ambao wanapenda mambo ya Sanda hayo, wakawa wameniuliza kuwa ninasemaje,  mbele ya Covid hii mbele ya SANDA YA TORINO.  Basi mimi nikaandika katika kavideo hivi: nikatuma kwamba mimi kuhusu hiyo SANDA YA TORINO  kitu ambacho tumekwisha fanya, matokeo ni kuangalia SANDA YA TORINO” ambayo ndiyo hiyo KWAUSO. Ni shule kwa ajili ya jamii, kwa ajili ya watu wote ambao wanataka kujua vizuri na shule ambayo ni kwa ajili ya wale ambao wanahitaji.  Na hivyo ndivyo ilivyo kuwa, kwa hiyo, nilikuwa ninatafakari juu ya SANDA YA TORINO ambayo ni KITU, MATOKEO YA KUTAFAKARI SANDA TORINO,  kwa sababu leo hii, nimeiwasha hapo muone ni kitu gani hiki)... Mnajua ni Kwauso, ambayo ni shule yetu, lakini wengine labda hawajui, maana yake au kirefu chake kwamba ni “Kwa Heshima ya Uso Mtakatifu kwa Bwana wetu Yesu Kristo.” Uso ambao upo pale (ukutani) ikiwa ni kitu cha pekee, basi ndiyo sababu tumefanya namna hiyo, na yote hayo yanatufanya tumshukuru Mwenyezi Mungu na tuendelee kumuomba Carlo Acutis, ambaye sasa ni mtu wa nyumbani, ameingia Mbinguni na kutangazwa Mbinguni akisha kuwa rafiki yetu. Kwa maana hiyo, tukimuomba atatusaidia mara moja, tusiogope kumuomba, tusiogope kuyatekeleza yale ambayo yeye mwenyewe alikuwa anayapenda.

Uzinduzi wa jiwe la Msingi wa kujenga nyumba ya mapadre
Uzinduzi wa jiwe la Msingi wa kujenga nyumba ya mapadre

Nyumba ya Mapadre itaitwa: “Veronica”

Hiyo nyumba tulisema tutaiita  Veronica. Wakatoliki wanajua  kwamba wakati kwaresima, au siku yoyote ambayo mtu anachagua huwa tunasali Njia ya Msalaba na katika njia ya Msalaba kuna kituo cha Sita na pale tunasikia kwamba kulikuwa na mama mmoja anaitwa Veronica anamuona Yesu, anapelekwa Kalvario, na Askari ambao ni wakali wamekwisha mpiga, uso wake hautambuliki, basi, huyo mama, alishikwa na huruma, akapita katikati ya maskari hao bila kujali chochote kitakacho tokea kwake, na alimpangusa Yesu. Na Yesu anampatia zawadi ya kitambaa, japokuwa kitu hicho akikuandikwa katika Injili, lakini ni kitu cha mapokeo. Kwa kuhitimisha alisema “Nisirefushe sana, yote hayo yameandikwa kwenye kitabu, ambacho sasa sitakitumia, basi, nashukuru sana, na nadhani ni muda wa kumaliza, kusudi twende tumuombe  Padre atuwekee jiwe la msingi, ili kusudi baada ya hapa, tuanze kuchangamka, tuanze kuburudika, tuanze yote ambayo yanaambatana na sherehe za kawaida. Tumsifu Yesu Kristo. Asanteni.

Kubariki jiwe la Msingi
Kubariki jiwe la Msingi
Misa ya kushukuru kutangazwa kwa Mtakatifu Carlo Acutis
11 Septemba 2025, 16:00