2025.09.24 Tabora,Tanzania:Jubilei ya miaka 50 ya Askofu Mkuu Mstafu Paul Ruzoka wa Jimbo Kuu la Tabora in Tanzania. 2025.09.24 Tabora,Tanzania:Jubilei ya miaka 50 ya Askofu Mkuu Mstafu Paul Ruzoka wa Jimbo Kuu la Tabora in Tanzania. 

Ask.Mkuu Mstaafu Paul Ruzoka,miaka 50 ya Upadre:malezi ya viongozi wakuu wa Kanisa

Askofu Mkuu Ruzoka tangu apewe Upadre tarehe 20 Julai 1975 katika Parokia ya Mtakatifu Theresia wa Avila,Nyaronga,Jimbo Katoliki la Kigoma amelitumikia Kanisa kwa uaminifu, unyenyekevu na moyo wa kisadaka kwa miaka 50 kati ya hiyo,miaka 35 katika ngazi ya uaskofu:“Tunapongeza kwa dhati tukio hili la furaha,tukikumbuka huduma yako ya kichungaji kwa bidii na uaminifu,"nimatashii mema na salamu kutoka kwa Papa Leo XIV katika tukio hilo.

Na Sarah Pelaji – Tabora, Tanzania.

Katika tukio la kihistoria na la kipekee kwa Kanisa Katoliki Tanzania, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki Tabora, Mhashamu Paul Ruzoka, ameadhimisha Jubilei ya Dhahabu ya miaka 50 ya Daraja Takatifu ya Upadri, tarehe 21 Septemba 2025. Maadhimisho hayo yalifanyika katika viwanja vya Kanisa Kuu la Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu, Jimbo Kuu Katoliki Tabora, yakihudhuriwa na maelfu ya waamini kutoka ndani na nje ya nchi. Askofu Mkuu Ruzoka alipewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 20 Julai 1975 katika Parokia ya Mtakatifu Theresia wa Avila, Nyaronga, Jimbo Katoliki la Kigoma na tangu wakati huo amelitumikia Kanisa kwa uaminifu, unyenyekevu na moyo wa kisadaka kwa miaka 50  kati ya hiyo, miaka 35 katika ngazi ya uaskofu.

Jubilei ya Askofu Mkuu Mstaafu Ruzoka wa Tabora
Jubilei ya Askofu Mkuu Mstaafu Ruzoka wa Tabora

Ibada Takatifu ya Jubilei iliongozwa na Mjubilei Askofu Mkuu Mstaafu Paul Ruzoka, akishirikiana na Mwadhama Protase Kardinali Rugambwa, Askofu Mkuu wa sasa wa Jimbo Kuu Tabora, ambaye pia alitoa Homilia Takatifu. Ibada hiyo ilihudhuriwa na Maaskofu kutoka Tanzania, pamoja na wageni kutoka nchi jirani za Burundi na Rwanda, sambamba na waamini waliokusanyika kwa wingi kushuhudia na kumshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha na utume wa Askofu Ruzoka.

Jubilei ya miaka 50 ya  Upadre ya Askofu Mkuu Mstaafu Ruzoka wa Tabora
Jubilei ya miaka 50 ya Upadre ya Askofu Mkuu Mstaafu Ruzoka wa Tabora

Salamu kutoka kwa Papa Leo XIV

Katika tukio la kipekee lililojawa kwa furaha na heshima, Askofu Mkuu Paul Ruzoka alipokea hata salamu maalum kutoka kwa Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Baba Mtakatifu Leo XIV, kwa heshima ya Jubilei ya miaka 50 ya Upadre. Salamu hizo za Papa Leo XIV zilitiwa saini tarehe 2 Juni  2025 , Vatican  zilisomwa rasmi tarehe 21 Septemba 2025 na Mkuu wa Idara ya Liturujia kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padre Clement  Kihiyo. Katika ujumbe wake, Papa Leo XIV alimpongeza kwa moyo wa dhati Askofu Ruzoka kwa kutimiza miaka 50 ya huduma ya kipadri, akimtaja kama “Mpendwa Paul Ruzoka,” na akimkumbuka kwa heshima na shukrani kutokana na mchango wake mkubwa katika ujenzi wa Kanisa, kwanza katika Jimbo Katoliki Kigoma na baadaye akiwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Tabora.

Askofu Mkuu Mstaafu Ruzoka akiwa anawasha mshumaa
Askofu Mkuu Mstaafu Ruzoka akiwa anawasha mshumaa

“Tunapongeza kwa dhati tukio hili la furaha, tukikumbuka huduma yako ya kichungaji kwa bidii na uaminifu,” ilisomeka sehemu ya salamu hizo. Papa Leo XIV pia alimuombea Askofu Ruzoka neema na baraka za mbinguni akisema: “Tunamuomba Kristo Mchungaji Mwema Amjalie thawabu tele, faraja ya roho na kufurahia afya njema.” Katika hitimisho la salamu hizo, Papa alimkabidhi Askofu Ruzoka pamoja na ndugu zake wote baraka za kitume kwa maombezi ya Bikira Maria Mama Mtakatifu wa Mungu, Mtakatifu Yosefu mwenye usafi kamili, na kwa neema ya Mwenyezi Mungu.

Kardinali Rugambwa: Askofu Mkuu Ruzoka ni jasiri wa Imani na kutetea masikini

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Tabora, Mwadhama Protase Kardinali Rugambwa, amelialika Kanisa kumshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha na utume wa Askofu Mkuu Mstaafu Paul Ruzoka, ambaye mwaka huu wa Jubilei Kuu ya Mwaka 2025 mwaka wa mahujaji wa matumaini  anatimiza miaka 50 ya Upadri na huduma ya kiaskofu. Tumshukuru Mungu kwa jinsi alivyomlinda, akamuwezesha kutimiza utume huu kwa uaminifu. Alisema Kanisa la Tanzania na la Ulimwengu linampongeza na kumuombea baraka zaidi kutoka kwa Mwenyezi Mungu ili awe na  furaha, afya na thawabu anayostahili kwa kazi aliyoifanya. “Nasi tunajiunga naye katika kuenzi alichokifanya, ili utume wake uendelee kuzaa matunda kupitia maisha yetu kwa utukufu wa Mungu". Kardinali Rugambwa aliendelea kubainisha: “Leo ni  kilele cha Jubilei, ambayo ni hitimisho la maadhimisho yaliyozinduliwa mwezi Oktoba mwaka 2024, chini ya kauli mbiu iliyotolewa kutoka Waraka wa Mtume Paulo kwa Wathesalonike: “Furahini siku zote, ombeni bila kukoma, shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu.” (1 Wathesalonike 5:16-18).

Kardinali Rugambwa
Kardinali Rugambwa

Kardinali Rugambwa alimpongeza Askofu Mkuu Ruzoka kwa ujasiri na uaminifu wake katika kushuhudia imani ya Kristo. Alilifundisha na kulitangaza Neno la Mungu "wakati ufaao na usiofaa", akikaripia, akiweka wazi na kuonya kwa uvumilivu mwingi na mafundisho ya kweli (2 Timotheo 4:2). Kama mwalimu na nabii, alisimama imara kutetea haki na kusimamia maadili katika maeneo mbalimbali aliyotumikia  ikiwemo Kigoma na Tabora. Aliwatetea wanyonge na masikini walioporwa haki zao kwa sababu ya kukosa uwezo wa kifedha au ushawishi. Alijitoa kuona kuwa waliodhulumiwa wanapata upendo wa Kristo kupitia huduma na sauti yake. Miongoni mwa mambo muhimu aliyoyasimamia ni: Ibada kwa Bikira Maria, kusimamia ukweli bila kuyumbishwa na kueleza mambo kwa uwazi bila kushinikiza.

Salamu za pongezi kutoka TEC

Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Mhashamu Eusebius Nzigilwa, alitoa salamu za pongezi kwa niaba ya TEC na waamini wote wa Kanisa Katoliki nchini. Alimpongeza Askofu Ruzoka kwa miaka 50 ya huduma ya upadri, akieleza kuwa maisha na utume wake yamekuwa baraka kubwa kwa majimbo ya Kigoma, Tabora, na Kanisa zima la Tanzania. Aliyapongeza mafanikio ya Askofu Ruzoka katika nyanja ya kichungaji, kiroho na kijamii, hasa kupitia mchango wake katika Baraza la Maaskofu, ambapo alihudumu kwa miaka 23 kama Mwenyekiti wa Tume ya Haki na Amani. Katika nafasi hiyo, alikuwa sauti ya kinabii akitetea utu, haki, upatanisho, na amani nchini.

Salamu kutoka kwa Askofu Nzigilwa,Makamu wa TEC
Salamu kutoka kwa Askofu Nzigilwa,Makamu wa TEC

Mchango wake Kitaifa na Kimataifa

Askofu Mkuu Msataafu Ruzoka amehusishwa na mafanikio mbalimbali ya kijamii na kisiasa nchini Tanzania. Kupitia tume ya Haki na Amani, TEC ilitoa maandiko muhimu kama Golden Opportunity (2008) na The One Billion Dollar Question, yaliyochangia kwa kiasi kikubwa katika mabadiliko ya sheria za madini nchini mwaka 2017. Aidha, aliwahi kushiriki katika kuunda Kamati ya Kidini ya Kusimamia Haki za Kiuchumi na Hifadhi ya Mazingira (ISCJIC), inayojumuisha TEC, CCT, na BAKWATA. Kamati hiyo ilitoa mapendekezo muhimu kwa serikali kuhusu mfumo wa kodi, uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali za taifa. Askofu Ruzoka pia anatambuliwa kwa mchango wake katika malezi ya viongozi wakuu wa Kanisa Katoliki Tanzania. Miongoni mwa waliopitia malezi yake ni Mwadhama Protase Kardinali Rugambwa, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dodoma Mhashamu Beatus Kinyaiya, na Balozi wa Papa (Nuncio) Mhashamu Novatus Rugambwa (sasa ni marehemu) na Makamu wa Rais wa Jmhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Philip Mpango ambapo  wote walilelewa naye katika Seminari Ndogo ya Itaga, ambapo alikuwa mwalimu wa Historia.

Zawadi Maalumu kutoka Jimbo Kuu la Tabora

Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki Tabora, Mhashamu Josaphat Bududu, alitangaza kwamba Jimbo limetoa zawadi ya ujenzi wa jengo jipya katika Seminari Ndogo ya Jimbo litakalobeba jina la Askofu Mkuu Paul Ruzoka kwa heshima yake. Aidha, jimbo limeweka kiasi cha fedha  katika akaunti yake ya  benki kwa ajili ya kumsaidia kuendelea na utume kama Askofu Msaafu ingawa kiasi cha fedha hakikutajwa.

Askofu Bududu , Msaidizi wa Jimbo Kuu la Tabora
Askofu Bududu , Msaidizi wa Jimbo Kuu la Tabora

Neno la Shukrani Kutoka kwa Askofu Ruzoka

Katika hotuba yake ya shukrani, Askofu Ruzoka alimshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai na wito wa upadri, akiwashukuru wazazi wake, walimu wa seminari, maaskofu na mapadre na wafadhili  wote waliomsaidia kufikia hatua hiyo ya miaka 50 ya huduma ya Upadre. Aliwaalika wote kuungana naye kumshukuru Mungu kwa neema hiyo  na kusisitiza haja ya kuendelea kusali kwa ajili ya afya ya roho na mwili ili kuendelea kumtumikia Mungu kwa uaminifu hadi mwisho, kwa matumaini ya kuufikia uzima wa milele. Maadhimisho hayo ni ushuhuda wa maisha ya utume wa upendo, huduma na kujitoa kwa ajili ya watu wa Mungu. Askofu Mkuu Mstaafu Paul Ruzoka amekuwa nguzo ya imani, haki na matumaini si kwa Kanisa tu, bali pia kwa taifa la Tanzania. Tunamuomba Mungu aendelee kumjalia afya, furaha na maisha marefu, na zawadi ya uzima wa milele. Hongera Askofu Mkuu Paul Ruzoka kwa Jubilei ya Dhahabu ya Upadri.

Wasifu wa Askofu Mkuu Mstaafu Paul Ruzoka

Alizaliwa Novemba 10 mwaka 1948 katika Kijiji cha Nyakayenzi kilichopo Wilaya ya Kankonko Mkoa wa Kigoma. Ni mtoto wa Pili kati ya watoto wa saba wa Mzee Bartholomeo Ruzoka Rubondo na Sidonia Bigina. Watoto watano walikwisha tangulia mbele ya haki, mpaka sasa wamebaki watoto wawili tu ambao Leonia Twezi na Paulo Ruzoka. Alipokea Sakaramenti Takatifu ya Ubatizo, Komunyo ya Kwanza pamoja na Sakramenti ya Kipaimara tarehe 1 Septemba 1960 katika Parokia ya Mt. Theresia wa Mtoto Yesu , Kankoko Jimboni Kigoma. Alipata elimu ya Msingi katika shule ya msingi Muhange iliyopo katika kijiji cha Muhange kati ya mwaka 1957 hadi 1960 kisha akijiunga na Seminari ndongo ya Mt. Yosefu, Ujiji mwaka 1961 -1965 wakati huo ziliitwa shule za kati (middle school). Mwaka 1966 – 1969 alijiunga na Seminari Ndogo ya Mt. Karoli Boromeo Itaga kwa masomo ya sekondari.

Mwaka 1970- 1971 alijiunga na Seminari Kuu ya Mt. Anthony wa Padua  Ntungamo Bukoba kwa masomo ya Falsafa. Mwaka 1972-1975 alijiunga na Seminari Kuu ya Kipalapala  Tabora kwa ya Masomo ya  Teolojia (Taalimungu). Baadaye alihitimu na kupata stashahada ya Teolojia kutoka Chuo Kikuu  cha Makerere Uganda. Alipata Daraja Takatifu la Ushemasi tarehe 21 Julai 1974 Katika Parokia ya Mt. Theresia  wa  Mtoto Yesu Muhange Kigoma na badaye alipata Daraja Takatifu la Upadre katika Parokia ya Mtakatifu Theresia wa Avila Nyaronga huko Jimboni Kigoma kwa mikono ya Askofu Daniel Nsabi.

Maaskofu walioshiriki Misa ya Jubilei huko Tabora
Maaskofu walioshiriki Misa ya Jubilei huko Tabora

Tarehe 7 Disemba 1989 aliteuliwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Kigoma kufuatia kifo cha Askofu Alphonce Daniel Nsabi. Tarehe 6 Januari 1990  aliwekwa wakfu katika Daraja Takatifu ya Uaskofu  kwa mkono wa Papa Yohane Paulo II (sasa ni Mtakatifu)  huko Mjini Roma, Italia. Alisimikwa rasmi kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Kigoma tarehe 25 Februari 1990 na Mkumbukwa Askofu Mkuu Mario Abdallah  Mgulunde aliyekuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Tabora wakati huo. Alilitumikia Jimbo Katoliki Kigoma kwa miaka 17.

Baada ya kifo cha aliyekuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Tabora Hayati Askofu Mkuu Mario Abdalla Mgulunde tarehe 14 Machi 2006, Baba Mtakatifu Benedikto XVI alimteua Askofu Paulo Ruzoka  kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Tabora tarehe 28 Januari 2007, akiwa ni Askofu wa nane wa Jimbo Kuu Katoliki Tabora na Askofu Mkuu wa nne na Askofu wa tatu mzalendo tangu kuingia kwa ukristo Jimboni Tabora.

Askofu Mkuu Mstaafu Ruzoka akiwa na ndugu yake
Askofu Mkuu Mstaafu Ruzoka akiwa na ndugu yake

Utume wa Upadre katika Kanisa na Jamii

Tarehe 13 Agosti hadi  30 Desemba  1975 alikuwa anahudumia Parokia ya Mt. Maria Kibondo, Kigoma kabla ya kuhamishiwa Seminari Ndogo ya Mt. Karoliki Boromeo Itaga Tabora kuwa mwalimu na mlezi. Alikuwa mwalimu na mlezi wa muda kwa miaka miwili katika Seminari Ndogo ya Itaga tarehe 7 Januari 1976 kabla hajajiunga na Chuo  cha Ualimu Chang’ombe ambako alitunukiwa Stashahada ya Elimu mwaka 1979. Alirudi seminarini Itaga kufundisha kabla ya kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) katika kambi ya Msange Tabora. Alikuwa mwalimu wa Historia, Kiswahili, Kingereza, Dini na Uraia kwa madaraja yote.

Baada ya kulitumikia Taifa alirudi tena Seminarini Itaga ambapo aliteuliwa kuwa Gambera wa Seminari (Rector) tarehe 7 Septemba 1980. Alifanya utume huo mpaka mwaka 1989 alipoteuliwa kuwa Askofu Mteule wa Jimbo Katoliki Kigoma. Alikuwa Mlezi wa Kiroho wa Jeshi la Milambo (JW) na katika kambi ya Msange (JKT). Aliwahi kuwa Katibu wa Baraza la Seneti la Mapadri wa Jimbo Kuu Katoliki Tabora, Katibu wa Bodi ya Seminari za Ujiji na Itaga na baada ya kujiunga kwenye mafunzo ya Biblia na mafungo huko Yerusalemu, Israeli mwaka 1987. Pia amewahi kuwa Mkuu wa Tume ya Haki na Amani (TEC) kuanzia mwaka 1991-2014 pia Mjumbe wa Baraza la Lipapa la Haki na Amani 1995-2014 na kitengo cha wakimbizi cha kipapa.

23 Septemba 2025, 10:17