Rais Hakainde Hichilema na Mama Mutale Nalumango, tarehe 24 Agosti 2021 wameapishwa kuwa Rais na Makamu wa Rais wa Zambia. Rais Hakainde Hichilema na Mama Mutale Nalumango, tarehe 24 Agosti 2021 wameapishwa kuwa Rais na Makamu wa Rais wa Zambia. 

Rais H. Hichilema wa Zambia: Vipaumbe: Rushwa, Maendeleo na Amani

Ushauri kwa Rais Hakainde Hichilema wa Zambia katika uongozi wake, ajitahidi kutoa kipaumbele cha kwanza katika mapambano dhidi rushwa na ufisadi wa mali ya umma. Ajizatiti na kujikita katika mchakato wa kufufua uchumi wa Zambia na, kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na umoja wa Kitaifa kwa vitendo! Ni wakati muafaka Wazambia wote wafurahie utajiri wao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Bwana Hakainde Hichilema wa Chama Cha United Party for National Development (UPND), tarehe 24 Agosti 2021 akiwa kwenye Uwanja wa Mashujaa Jijini Lusaka ameapishwa kuwa ni Rais wa Saba nchini Zambia, baada ya Bwana Edgar Lungu kutoka katika Chama cha Patriotic Front (PF) kuridhia matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2021 na hivyo kumaliza rasmi muda wake wa uongozi. Mama Mutale Nalumango ameapa kuwa Makamu wa Rais wa Zambia. Rais Hakainde Hichilema amekagua gwaride la heshima na kupigiwa mizinga 21. Ndege za kivita zilikuwa zinarukwa utadhani mbayuwayu! Yote hii ni kuonegesha furaha ya watu wa Mungu nchini Zambia. Sherehe hizi zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka ndani na nje ya Bara la Afrika. Kati yao ni ujumbe wa Bostwana uliongozwa na Rais Mokgweetsi Masisi kati yao akiwamo Rais Mstaafu Festus G. Mogae wa Botswana pamoja na kiongozi wa Chama cha Upinzani Dr. Lemogang Kwape. Wachunguzi wa mambo ya kisiasa nchini Zambia wamefurahishwa sana na kitendo cha Hakainde Hichilema maarufu kama “HH” kuwaalika viongozi wa vyama vya upinzani kutoka kutoka Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, SADC.

Huu ni mwanzo mpya katika ujenzi wa umoja na udugu wa kibinadamu Barani Afrika. Ujumbe wa Tanzania ukiwa umesheheni viongozi wa Cham ana Serikali umeongozwa na Rais Rais Samia Suluhu Hassan akiwemo Mzee Mizengo Peter Pinda, Waziri mkuu mstaafu pamoja na Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete aliyekuwa kiongozi wa Timu ya Waangalizi wa Uchaguzi kutoka Jumuiya ya Madola. Rais Joseph R. Biden wa Marekani, amewakilishwa na ujumbe wa watu watatu! Askofu Charles Kasonde wa Jimbo Katoliki la Solwezi nchini Zambia amemshauri Rais Hakainde Hichilema wa Zambia katika uongozi wake kutoa kipaumbele cha kwanza katika mapambano dhidi rushwa na ufisadi wa mali ya umma. Kujikita katika mchakato wa kufufua uchumi wa Zambia na hatimaye, kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na umoja wa Kitaifa kwa vitendo! Amewashukuru viongozi wa Awamu ya Sita waliomaliza uongozi wao. Walikuwa na mafanikio pamoja na madhaifu yao, sasa ni wakati wa kuganga na kuponya madhaifu haya. Huu ni wakati muafaka wa kuboresha miundo mbinu ya barabara hasa katika eneo la Kaskazini Magharibi wa Zambia, ili hata Wazambia wanaoishi katika maeneo haya waweze kufurahia rasilimali na utajiri ambao Mwenyezi Mungu amewakirimia Wazambia. Uchaguzi mkuu ulifanyika tarehe 12 Agosti 2021.

Baba Mtakatifu Francisko anasema rushwa ni mchakato unaoharibu na kuvunjilia mbali kabisa mafungamano, upendo na mshikamano wa binadamu. Rushwa inatia doa uhusiano kati ya binadamu, Mwenyezi Mungu na kazi ya uumbaji. Lakini kinyume cha rushwa ni: Uaminifu, uadilifu, utu wema, upole na unyoofu wa moyo mambo yanayopania kukuza na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Rushwa inaonesha maisha ya mwanadamu asiyekuwa na dira wala mwelekeo sahihi wa maisha, hali inayoharibu sana mafungamano ya kijamii. Matokeo yake ni kukomaa kwa uchoyo na ubinafsi usiokuwa na mvuto wala mashiko pamoja tabia ya kutowajali wengine. Rushwa inaonesha ile “roho ya korosho, roho ya kwa nini; roho ya kutu, roho iliyovunda na kuanza kutoa harufu mbaya”. Rushwa ni kikwazo katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Rushwa inapelekea kushamiri kwa biashara haramu ya binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo.

Rushwa ni chanzo kikuu cha kuibuka na kusambaa kwa magenge ya kihalifu, kitaifa na kimataifa. Haya ni magenge yanayochochea utamaduni wa kifo. Kimsingi, rushwa ni adui wa haki, utu na heshima ya binadamu.  Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, ili kupambana na rushwa pamoja na ufisadi kuna haja ya kuwajengea vijana uwezo wa kiuchumi, kimaadili, kitamaduni na kiutu! Hii inatokana na ukweli kwamba, rushwa inapata chimbuko lake katika moyo wa mwanadamu! Rushwa ina tabia ya kujigeuza geuza kadiri ya mazingira na vionjo vya mtu, kumbe, hakuna anayeweza kujidai kwamba, rushwa ameipatia kisogo! Dhana ya maendeleo fungamani ya binadamu inajikita katika mchakato mzima wa majadiliano katika ukweli na uwazi kwa kuangalia vipaumbele na mahitaji msingi ya binadamu na wala si kutazama soko la dunia. Huu ni mchakato wa ujenzi wa sanaa ya kusikiliza na kusikilizana; kwa kujikita katika kanuni maadili na utu wema katika masuala ya kiuchumi; kwa kutumia vyema rasilimali fedha na watu katika mchakato wa maisha ya watu wa Mungu.

Familia ya Mungu Barani Afrika haina budi kujizatiti kikamilifu, ili kukabiliana na changamoto za athari kubwa ya mabadiliko ya tabianchi, myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa, ili kukuza na kudumisha mshikamano unaofumbatwa katika kanuni auni ili hatimaye, kutangaza na kushuhudia Injili ya amani Barani Afrika kama chachu ya maendeleo fungamani kwa watu wa Mungu! Jamii ni mdau mkubwa wa mchakato wa uchumi fungamani. Ushirikishwaji huu unapaswa kuzingatia: mafao ya wengi, sheria, kanuni na taratibu kama sehemu muhimu sana ya utekelezaji wa haki pamoja na kusimama kidete katika misingi ya maendeleo, ustawi na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Francisko mintarafu uchumi anasema, kuna haja ya kupanua zaidi dhana ya haki kadiri ya Mapokeo kwa kuanzia katika mchakato wa uzalishaji na ugawanaji wa faida iliyopatikana. Katika masuala ya uzalishaji na huduma; wafanyakazi wanapaswa kupewa mshahara unaokidhi mahitaji yao msingi sanjari na kuzingatia: utu, heshima na haki zao msingi mintarafu kanuni maadili na utu mwema. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walikazia kwa namna ya pekee, kanuni na taratibu katika maisha ya kiuchumi na kijamii katika ujumla wake. Mfumo wa kazi hauna budi kuzingatia madai ya binadamu, maisha yake, dhamana na majukumu yake katika familia. Wafanyakazi wanawajibika kutumia muda, bidii na weledi katika mchakato mzima wa uzalishaji na utoaji huduma.

Wafanyakazi wapewe muda wa kupumzika na kushughulikia: ukuaji na ustawi wa familia zao. Mafundisho Jamii ya Kanisa kwa namna ya pekee, yanatoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na udugu wa kibinadamu kama kanuni msingi na kiini cha sera na mikakati ya kiuchumi. Udugu wa kibinadamu unakamilishwa na mshikamano badala ya kuzingatia tu tija katika mchakato mzima wa uzalishaji. Udugu wa kibinadamu kiwe ni kipimo cha mahusiano na mafungamano ya kijami. Udugu ni dhana inayofumbatwa katika Maandiko Matakatifu kwa kukazia anasema Baba Mtakatifu mshikamano wa dhati unaotambua na kuthamini uwepo wa jirani, utu na heshima yao; uhuru na haki zao msingi pamoja na ushiriki wao katika mchakato mzima wa mafao ya wengi kadiri ya nafasi, uwezo, wito, mpango wa maisha na karama katika huduma.

Kwa bahati mbaya, ni watu wachache sana ambao wamesikiliza na kutambua matatizo ya uchumi mamboleo kiasi hata cha kuthubutu kuweka mifumo mipya ya uchumi ambayo ni matunda ya utamaduni wa umoja unaojikita katika udugu wa kibinadamu na usawa. Mtakatifu Francisko wa Assisi ni mfano bora wa kuigwa katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote sanjari na ikolojia fungamani. Ni Mtakatifu Francisko aliyethubutu kufanya ukarabati mkubwa wa “Nyumba ya Mungu” iliyokuwa inaporomoka. Huu ni wajibu wa watu wote yaani: Kanisa, jamii na kwa kila mtu binafsi. Utunzaji bora wa mazingira unahitaji uchumi makini na maendeleo fungamani yanayoweza kuponya madonda, na hivyo kuwahakikishia watu matumaini kwa siku za mbeleni. Ili kuweza kutekeleza kwa dhati changamoto hii, kuna haja kwa kila mtu kuanza kufikiri na kujikita katika kanuni maadili, Amri za Mungu na mafao ya wengi.

Rais Zambia

 

24 August 2021, 14:41